News and Resources

New Water Use Fees

Ada Mpya za Matumizi ya Maji
Ada za Matumizi ya Maji na Ada nyingine zinazotozwa na Bodi za Maji za Mabonde ziliwekwa kwa mujibu wa Kifungu Na. 38 (2) cha Water Utilization Act Na. 42 ya mwaka 1974 na marekebisho yake ya mwaka 2002 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 256 la tarehe 21 Juni 2002. Hadi sasa imepita takribani miaka 10 tangu viwango hivyo vya ada vilipoanza kutumika. Kutokana Na kuongezeka kwa gharama za usimamizi, uratibu Na uendelezaji wa Rasilimali za Maji, kiwango cha ada zinazotozwa na Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani kwa sasa hazitoshi kuchangia katika kuboresha huduma ya maji na kusimamia matumizi bora ya rasilimali hii muhimu, kuelimisha watumiaji wa maji kuhusu Sheria za Maji na hifadhi ya mazingira.

Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani kwa mamlaka iliyopewa chini ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Namba 11 ya Mwaka 2009 Kifungu cha (96) inatangaza viwango vipya vya ada za matumizi ya maji na ada zingine. Viwango hivi vimeandaliwa kwa kuzingatia muongozo wa Wizara ya Maji na vitatumika katika kipindi cha mpito hadi hapo Wizara ya Maji itakapotoa maelekezo mengine ya kupanga viwango halisi vya kutumika. Kutangazwa kwa viwango hivi vya ada za matumizi ya maji na ada nyingine kunafuta ada za viwango vya zamani vilivyotangazwa kwenye gazeti la Serikali Na. 256 la tarehe 21 Juni 2002. Viwango vinavyotangazwa vimeambatishwa hapa chini kama vilivyoidhinishwa na Wizara ya Maji pamoja na tangazo la Bodi ya Maji Bonde la Pangani kwenye magazeti ya Daily News na Mwananchi ya tarehe 29 Mei 2014.